DAR ES SALAAM: Mtiti! Msanii
nyota wa Muziki wa Kizazi Kipya, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ wikiendi
iliyopita alitoa kali ya mwaka, baada ya kuzichapa kavukavu na mlinzi
‘baunsa’ wa pool party yake iliyofanyika katika eneo la ofisi ya BKT
iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam, baada ya kumfanyia ‘kauzibe’.
ILIVYOKUWA AWALI
Shilole, ambaye ni balozi wa kondomu
zinazofahamika kama Bulls Mpe Raha, alikuwa amefanyiwa sherehe na
kampuni inayosambaza bidhaa hiyo ili aburudike yeye pamoja na watu wake
wa karibu, sambamba na wadau wengine wa ‘menejimenti’ hiyo.
Kama mtu mwenye shughuli, msanii huyo
anayejisifu kwa uamuzi wake wa kutoka na ‘vijana wadogo’, aliwaalika
baadhi ya watu wake wa karibu, wakiwemo wasanii wenzake na kuifanya pati
hiyo kuwa yenye kuvutia, kwani vyakula na vinywaji halikuwa jambo la
kuuliza.
Ilipofika saa saba za usiku, Shilole
alitaka kuondoka kwenye pati hiyo ili awahi katika shoo, ambayo
alitakiwa kuifanya katika Ukumbi wa Billicanas uliopo katikati ya jiji,
yeye na Vanessa Mdee ‘Vee Money’.
Lakini kwa vile vinywaji vilikuwa bado
vingi na yeye hakuwa ametosheka, alimuomba mtu aliyeonekana bosi wa
kampuni hiyo, aruhusiwe kubeba bia zisizohitajika kurejesha chupa (take
away), kitu ambacho kilikubalika na mkali huyo wa Kibao cha
Nyang’anyang’a akajisevia chupa zipatazo kumi za bia za bei mbaya tayari
kwa kusema.
AKUTANA NA BAUNSA GETINI
Getini, staa huyo ambaye pia anajulikana
kama Shishi Baby, akakutana na baunsa aliyetoa maneno ambayo Shilole
alitafsiri kama yenye kumdhalilisha.
“Hamna kutoka na bia hapa, watu wote
tumewazuia kuondoka na bia, kwani wewe ni nani hasa, hizo chupa kesho
tuna kazi ya kuzihesabu,” alisema baunsa huyo.
Shilole akiwa amepigwa na butwaa, alijitahidi kumuelewesha kistaarabu sababu za yeye kuchukua bia.
“Sikia kaka, hii shughuli ni yangu, watu
wote hapa wamekuja kwa sababu yangu na isitoshe, hizi ni take away
(chupa zisizohitajika kurudishwa), halafu pia nimemuomba meneja na
ameniruhusu, wewe nani unanizuia?”
Baunsa huyo aliyefahamika kwa jina moja
la Mansuri, hakuelewa somo, akashikilia msimamo wake, licha ya baadhi ya
wadau walioanza kukusanyika, kumsihi atumie busara.
HALI YA HEWA YACHAFUKA, PACHIMBIKA
Baada ya Shilole kuona ‘saundi’ zake
hazina msaada, akaamua kujilipua, liwalo na liwe kwa kuanzisha vurugu
akilazimisha kutoka na vinywaji vyake, jambo lililosababisha wawili hao
kuchapana vibao.
Wadau waliokuwa karibu na tukio hilo
walisogea na kutaka kuingilia kati, lakini Shilole alikuwa mkali, jambo
lililosababisha wasamaria wema hao kupata wakati mgumu kuwaamulia.
Hata hivyo, baadaye walifanikiwa kuamua ugomvi huo, uliomuacha Shilole akiwa hoi kwa uchovu uliochanganyika na kinywaji.
SHILOLE ALONGA
Baada ya timbwili hilo, msanii huyo
alionesha mshangao wake kwa mlinzi huyo, baada ya kuliambia gazeti hili
kuwa ni jambo la kushangaza kuona mtu ambaye hafahamu umuhimu wake
katika kampuni anayoitangaza, kumzuia kuondoka na bia.
“Mimi ndiyo mara yangu ya kwanza kuwa
balozi na nimeanza kazi vizuri, nashangaa mtu anataka kuniharibia wakati
hata hahusiki, hawa watu wote hapa nimewaalika mimi, leo mtu haoni.
“Hata kama chupa zile zinahesabiwa kesho yake, kwani si angesema nilichukua mimi, kulikuwa na tatizo gani?” alisema.
0 comments:
Post a Comment