NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji amesema baadhi ya wafanyabiashara nchini wamekuwa wakitumia kisingizio cha mtandao kukwepa kutoa risiti za kielektroniki (EFDs) na kuonya kuacha tabia hiyo mara moja.
Alisema tabia hiyo imejijenga miongoni mwa wafanyabiashara na kuwa
kwa sasa serikali inafanya jitihada kuhakikisha suala hilo haliwi
kisingizio.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Neema Mgaya
(CCM) aliyetaka kufahamu serikali inakabiliana vipi na changamoto ya
mtandao ambayo inakwamishwa na baadhi ya wafanyabiashara kutoa risiti za
kielektroniki.
“Niwatake wafanyabiashara kuacha danganyatoto wahakikishe wanatoa
risiti za kielektroniki kwani suala la mtandao sio tatizo ndio maana
hata mabenki yanafanya kazi zao vizuri,” alisema Dk Kijaji.
Aidha, Kijaji amesema mpaka sasa wafanyabiashara 118 katika Jiji la
Dar es Salaam wenye mtaji mdogo waliotakiwa kuchukua mashine za EFDs
ndio waliochukua mashine hizo.
Alisema serikali imetenga mashine zipatazo 5,703 kwa ajili ya
wafanyabiashara wenye mitaji midogo na kuwataka wafanyabiashara hao
kwenda kuchukua mashine hizo.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Mgonokuliwa
(CCM) aliyetaka kufahamu kama kulikuwa na ushirikishwaji kati ya
waandaji wa mfumo wa TRA na viongozi wa wafanyabiashara ili kodi
inayotozwa iwe halali na isiwe inayoua mitaji ya wafanyabiashara.
Akijibu swali hilo, Dk Kijaji alisema hakuna kodi inayotozwa kwa nia
ya kuua mitaji ya wafanyabiashara kwani kiwango cha kodi ya mapato ni
asilimia 30 ya mapato baada ya kuondoa gharama za biashara.
“Pale ambapo mfanyabiashara hakupata faida, hakuna kodi ya mapato
inayotozwa, kodi zinazotozwa na TRA ni halali na haiui mitaji ya
wafanyabiashara wetu,” alisema.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema azma ya
serikali ni kuhakikisha inajenga ofisi za TRA katika kila mji ili
kuongeza ukusanyaji.
Alitoa kauli hiyo wakati wa kujibu swali la nyongeza la Mbunge Kasulu
Mjini, Daniel Nsanzugwanko (CCM) aliyetaka kufahamu serikali itajenga
lini ofisi ya TRA katika mji wa Kasulu ukiwa ni mji wa kibiashara.

0 comments:
Post a Comment