.

.

10,000 waajiriwa na kampuni ya SAGCOT

Mwenyekiti wa Bodi ya SAGCOT, Balozi Ami Mpungwe
Mwenyekiti wa bodi ya SAGCOT, Balozi Ami Mpungwe
KAMPUNI tano zilizopata ufadhili wa fedha kutoka katika Mfuko Kichocheo wa Ukanda wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) zinatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 10,000 zitakapoanza utekelezaji wa miradi yao.
Zilipata ufadhili wa dola za Marekani 3,915,950 (Sh bilioni 8.2) zinatarajiwa kuzalisha ajira rasmi za moja kwa moja zipatazo 4,330 na nyingine 8,520 katika mnyororo wa thamani.
Hayo yalielezwa juzi na Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo, Balozi Ami Mpungwe kwenye hafla ya utilianaji saini wa mikataba ya ufadhili wa fedha katika mfuko huo na kampuni hizo zilizoomba ufadhili.
Alitaja kampuni zilizopata ufadhili huo ni pamoja na kiwanda kidogo cha sukari cha Geoman Cane Estate Ltd, kiwanda cha maziwa cha Asas, kiwanda cha maziwa cha Njombe, kampuni ya Muvek Development Sln Ltd na Mtenda Kyela Rice Ltd.
“Tunategemea uzalishaji wa mazao ya mpunga, maziwa, sukari, mayai na kuku wa kienyeji utaongezeka kutokana na kujenga miundombinu sahihi kwa wakulima na wafugaji wadogo pamoja na kuwajengea uwezo na mbinu za kuzalisha kulingana na mahitaji ya soko,” alisema Balozi Mpungwe.
Akizungumza wakati wa kufungua hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joel Malongo alisema, serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji hasa katika sekta ya viwanda ili kufikia ajenda ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.
Malongo aliyemwakilisha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema, Sagcot inafanya kitu kikubwa ambacho kinaiunga mkono Serikali ya Awamu Tano hasa katika sekta ya viwanda.
“Lakini pamoja na hayo tunatambua kuna changamoto nyingi, sisi kama Wizara tunajaribu kuzungumza na wenzetu ili kutatua changamoto mbalimbali ikiwa ni kurahisisha mazingira ya uwekezaji,” alisema Malongo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko huo, John Kyaruzi alisema, lengo kubwa ni kuamsha kilimo cha biashara kwa kumuunganisha mkulima mdogo na masoko ili aweze kunufaika kupitia kilimo.
Alisema wakulima wengi nchini wanakabiliwa na matatizo makuu matatu ambayo ni kushindwa kukidhi viwango vya soko, kutokuwa na masoko ya uhakika na matatizo ya kibiashara.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba wa ufadhili huo, Mkurugenzi Mtendaji Geoman Cane Estate Ltd, Dk George Mlingwa alisema baada ya kupata fedha hizo anatarajia kuanza ujenzi wa kiwanda kitakachokamilika kabla ya msimu huu kumalizika.
Alisema ujenzi huo utagharimu dola za Marekani milioni mbili (Sh bilioni 4.5) na kitagharimu Sh bilioni nane kikijumuisha shughuli nyingine zikiwemo za mashamba. Alisema kiwanda hicho kitanufaisha wakulima takribani 500.
Share on Google Plus

About UPStream Telecom

0 comments:

Post a Comment