Alisema hatua hiyo ya kuongeza fedha za bajeti kwa sekta ya afya itawezesha Tanzania pamoja na nchi nyingine zinazoendelea za Afrika kuboresha eneo la utafiti litakaloweza kuibua masuala nyeti yanayogusa moja kwa moja jamii.
Akifungua Mkutano wa Nne wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) unaohusu masuala ya Mafunzo na Sayansi, Samia alisema tayari katika bejeti ya 2016/17 serikali imejitahidi kuongeza kiwango cha fedha katika sekta hiyo, ingawa bado hakijafikia asilimia 15 kama ilivyoridhiwa.
“Nichukue fursa hii kuwahakikishia kuwa Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa sekta ya afya lakini pia inatambua mchango mkubwa wa utafiti unaofanywa na wataalamu wa afya. Nawahakikishia katika bajeti zetu zijazo serikali itahakikisha asilimia hii 15 inafikiwa,” alisisitiza.
Katika bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni ilikuwa ni Sh bilioni 845 ambayo ni chini ya asilimia 10 ya bajeti nzima ambayo ni Sh trilioni 29.
Aidha, aliwataka wataalamu wa masuala ya afya nao kuondokana na utegemezi wa misaada kutoka kwa fadhili katika utekelezaji wa miradi muhimu ikiwemo masuala ya utafiti kutokana na ukweli kuwa misaada mingi huwa na muda wa kukatishwa na hivyo huenda malengo ya mradi husika yasifikiwe.
Aliushauri uongozi wa MUHAS kujenga uhusiano wa karibu na viwanda vya ndani na kimataifa kwa ajili ya kuimarisha eneo la utafiti na mafunzo. Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Muhas, Profesa Ephata Kaaya alisema chuo hicho tangu kianzishwe miaka 50 iliyopita, kimefanya utafiti mbalimbali ambao umesaidia kuiwezesha wizara kutunga sera zinazoendana na hali halisi kwa mfano Sera ya Ukimwi na Malaria.
0 comments:
Post a Comment