KAMPUNI ya utoaji mikopo ya Yetu, imesema inatarajia kutumia Sh bilioni mbili kuwanufaisha wakulima nchini kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha kisasa.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Dar es Salaam kwenye mafunzo ya kilimo kwa wadau mbalimbali, Mkurugenzi Mtendaji wa Yetu, Altemius Millinga alisema fedha hizo zitatumika kutoa elimu na mikopo kwa wakulima watakaokuwa tayari kuendeleza kilimo hicho.
Alisema kwa kuanza wanatarajia kusaidia wakulima 200 katika kipindi cha mwaka mmoja, utakaomalizika Julai mwakani.
Millinga alisema katika kuanza utekelezaji huo, wameanza mafunzo kwa wadau 32 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kigoma na Ruvuma kujifunza mbinu za kupata mikopo, kuendeleza kilimo, namna ya kujenga nyumba ya kitalu na umwagiliaji wa matone.
“Lengo la kuandaa mafunzo haya, tunataka kuwajenga wakulima kuchagua kilimo cha kisasa cha nyumba ya kitalu, kuondokana na kilimo cha mazoea,” alisema.
Alisema pia wanataka kutoa mikopo kwa wakulima wadogo na kuona kuwa kilimo cha kisasa kinawezekana.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya usambazaji ya zana za nyumba za kitalu ambao wanashirikiana na Yetu katika mafunzo hayo, Joseph Kadendula alisema kilimo hicho cha kisasa ni mkombozi kwa mkulima.
Alisema ni mkombozi kwa kuwa hakiwezi kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na kina uwezo wa kutumia maji kidogo na eneo dogo kupata mazao mengi yanayoendelea kuzaa.
Kadendula alisema gharama ambazo hutumika kwa kujenga nyumba moja ya kitalu huanzia Sh milioni saba hadi 15, kutegemeana na aina ya vifaa na mahitaji ya mazao.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka Asasi ya kiraia ya Kilimo na Biashara, Eric John alisema mafunzo waliyopata watayachukua kuendeleza kilimo katika hekta 500 wanazotarajia kulima.
0 comments:
Post a Comment