Na Gladness Mallya, UWAZI
DAR
ES SALAAM: Ni shida! Mtoto Zainabu Shaban, 16, (pichani) mkazi wa
Kimara-King’ong’o, Dar amejikuta katika wakati mgumu baada ya kudaiwa
kuvunjwa mguu na baba yake mzazi wakati wakiwa kwenye ugomvi na mama
yake kisa kikitajwa mchepuko.
Akizungumza na gazeti hili, Zainabu alidai siku ya tukio baba na mama
yake walikuwa wana ugomvi akaamua kukimbilia kwa jirani yao ambapo
alilala huko na kurudi nyumbani kesho yake na kujiandaa kwenda shule
kwani anasoma kidato cha pili.
Jioni alirudi nyumbani na kumkuta baba yake akiwa ameandaa fimbo kwa
ajili ya kumchapa kisa, jana yake alikwenda kulala kwa jirani hivyo
alipoingia tu ndani alimpokea na kumtaka alale chini ili amuadhibu,
akatii amri hiyo ikawa anachapwa ndipo mama yake alipoingilia kati baada
ya kuona anaumizwa kwa sababu fimbo ilikuwa kubwa.
“Mama aliingilia ambapo baba alimgeukia na kumpa kipigo ikabidi
ninyanyuke pale nilipokuwa nimelala na kuwaamua, baba akanigeukia tena
kutaka kunipiga ikabidi nikimbie lakini nilijikwaa kwenye mlango naye
akaja akanikanyaga mguu, ukavunjika, kiukweli naumia sana na sitaki hata
kumuona baba maana amenipa kilema,” alidai Zainabu.
Zainabu akiwa na mama yake.
Naye Mama Zainabu alieleza kuwa mumewe ndiye aliyemvunja mtoto wao mguu
na ilikuwa ni kwenye ugomvi kati yake na mumewe baada ya kumwambia
aachane na mchepuko ambao unamzuia kutoa matumizi muhimu kwa watoto
wanne. “Ugomvi na mume wangu umekuwa ni wa kila siku sababu kubwa ni
kwamba ana mchepuko na mwanamke mwenyewe namfahamu na hivi karibuni
niliwafuma nikamshushia kipigo sana huyo mwanamke, hatoi matumizi
nyumbani na mara mojamoja ndiyo anaacha shilingi elfu mbili ambazo
hazitoshi chochote, amemvunja mwanangu mguu lakini hataki hata
kumhudumia, nauza matembele ndiyo napata nauli ya kumpeleka Hospitali ya
Muhimbili.
“Mume wangu siku ya ugomvi nilimshauri tu aachane na huyo mwanamke kwani
kama kipato chake ni kidogo anapata wapi fedha za kumpa, ndipo ugomvi
ulipoanzia na kusababisha matatizo yote haya.
“Alikamatwa na polisi akakaa huko siku kadhaa nikaenda kumwekea dhamana
ili tuje kusaidiana matibabu lakini hakuna anachonisaidia,” alidai mama
huyo.
Baba wa mtoto huyo, Shaban alipotafutwa alikiri kutokea kwa ugomvi huo
na kumpiga mwanaye lakini suala la kumvunja mguu alikanusha.
“Mke wangu anasema uongo, huyo mtoto alianguka mwenyewe wakati anakimbia
nisimchape, kipato changu ni kidogo na matumizi ya nyumbani natoa
lakini mke wangu haridhiki na hicho kidogo, naumia sana
wanavyonisingizia nimemvunja mguu mtoto wangu na kuwa na mchepuko,”
alisema Shaban.
Mwenyekiti wa mtaa wa eneo hilo, Demetrius Mapesi alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo. “Mtuhumiwa yaani baba wa Zainabu alifikishwa katika
Kituo cha Polisi Kimara na kufunguliwa kesi namba KMR/RB/1822/2016
KUSHAMBULIA, lakini baadaye alitolewa kwa dhamana,” alisema.
0 comments:
Post a Comment