Rais John Magufuli
SIKU chache baada ya uteuzi wa wakuu wa wilaya, Jukwaa Huru la
Wazalendo Tanzania limeeleza kufurahishwa na namna Rais John Magufuli
anavyozidi kujipambanua kwa Watanzania kuwa Rais wa Watanzania wote bila
kujali itikadi za kisiasa.
Katibu wa Jukwaa hilo, Mtela Mwampamba akizungumza Dar es Salaam jana
alisema uteuzi wa wakuu wa wilaya umezingatia uadilifu, uwajibikaji,
uzalendo na uwezo wa kiongozi husika katika kuwaunganisha wananchi.
“Jukwaa linatumia fursa hii kumpongeza Rais kwa uteuzi wa wakuu wa
wilaya alioufanya hivi karibuni. Rais amezidi kudhihirisha kuwa yeye ni
kiongozi anayeishi na kusimamia kile anachoahidi kwa vitendo.
“Rais alisema na namnukuu; ‘Nimeona vijana ndio wachapakazi,
wasiopenda rushwa na wazalendo, hivyo nitaendelea kuwaamini ndani ya
serikali yangu kwa kuwateua kunisaidia kazi mbalimbali’, mwisho wa
kunukuu.
“Hili amelitimiza na kulithibitisha katika uteuzi huu wa wakuu wa
wilaya ambapo kwa zaidi ya asilimia 70 ya wateuliwa wote ni vijana. Sote
tunajua vijana wana ari, utayari na shauku ya kuongoza kwa sifa ya
kiuongozi ambazo ni uadilifu, ubunifu, uwajibikaji na uzalendo."
Alisema jukwaa hilo linatoa rai kwa Watanzania, viongozi wa dini na
kisiasa kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli katika harakati za kuleta
maendeleo.

0 comments:
Post a Comment