MAMBO bado si mazuri kwa Yanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho
la Soka Afrika (CAF CC) baada ya jana kukubali kipigo cha bao 1-0
kutoka kwa TP Mazembe.
Hicho ni kipigo cha pili mfululizo kwa Yanga katika michuano hiyo
baada ya Juni 19 mwaka huu kufungwa idadi kama hiyo ya bao ugenini na MO
Bejaia ya Algeria.
Kutokana na mazingira hayo Yanga inabidi ifanye kazi zaidi katika
michezo iliyobaki ili kuhakikisha inafufua matumaini ya kufuzu nusu
fainali ya michuano hiyo.
Mchezo wa kwanza TP Mazembe iliifunga Medeama ya Ghana mabao 2-1
mjini Lubumbashi, DRC, hivyo kwa matokeo ya jana inaendelea kuongoza
kundi ikiwa na pointi sita.
MO Bejaia na Medeana zinatarajiwa kucheza leo.
Bao hilo pekee katika mchezo wa jana lilifungwa dakika ya 75 na
Merveille Bope, ambapo lilitokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Jean
Kilitcho na kumkuta Roger Asale aliyeupeleka kwa mfungaji.
Katika mchezo wa jana, ambao mashabiki waliingia uwanjani bila kulipa
kiingilio, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm alimuanzisha Juma Mahadhi
aliyesajiliwa kutoka Coastal Union ya Tanga na Obrey Chirwa raia wa
Zambia aliyetokea FC Platinums ya Zimbabwe.
Pia jana alicheza beki Juma Abdul aliyekosa mchezo uliopita dhidi ya
Mo Bejaia kutokana na kuwa majeruhi. Mahadhi aliipa uhai safu ya
ushambuliaji ya Yanga, ingawa suala la umaliziaji lilionekana kuwa
tatizo kubwa.
Washambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma, Chirwa na Deus Kaseke mara
kadhaa walifika kwenye lango la Mazembe ambao ni mabingwa wa Afrika wa
msimu uliopita, lakini walishikwa na kigugumizi na kushindwa kulenga
lango.
Katika mchezo huo Mazembe itajutia zaidi nafasi ilizopata dakika ya
5, 28, 53 na 60, zilizopotezwa kwa nyakati tofauti na Adam Traore,
Thomas Ulimwengu, Asale na Christiaan Nekadio.
Yanga haikufanya mashambulizi ya nguvu sana, lakini ilipata nafasi
nzuri zaidi ya dakika ya nane, ambayo haikutumiwa vyema na kiungo
Thabani Kamusoko.
Nao wachezaji Ngoma, Haruna Niyonzima, Chirwa na Mahadhi pia
waliingia mara kadhaa katika eneo la hatari, lakini walishindwa
kutumbukiza mpira wavuni.
Ni matokeo ambayo yalikuwa machungu kwa maelfu ya mashabiki wa Yanga
waliojitokeza uwanjani hapo kwa wingi kuishangilia timu yao, lakini
mambo hayakuwa walivyotarajia.
Yanga; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mbuyu Twite, Vincent Bossou,
Kevin Yondan, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Juma
Mahadhi/ Geoffrey Mwashiuya, Obrey Chirwa/Matheo Simon na Donald Ngoma.
TP Mazembe; Sylvain Gbohoud Guelassiognon, Jean Kasusula, Issama
Mpeko, Salif Coulibaly, Rodger Asale, Adama Traore/Deogratius Kanda,
Merveille Bope, Nathan Sinkala, Koffi Christian/Jose Bodibake, Christian
Luyindama na Thomas Ulimwengu.

0 comments:
Post a Comment