SHIRIKA lisilo la kiserikali la Pelum Association, limesema migogoro ya ardhi imeonekana kupungua katika maeneo mbalimbali wilayani Bahi, mkoani Dodoma kutokana na viongozi wa vijiji kuelewa umuhimu wa kusimamia ardhi ikiwemo kuacha kuiuza kiholela.
Ofisa Miradi wa shirika hilo, Anna Marwa alisema hayo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati za uamuzi wa ardhi wa wilaya ya Bahi.
Alisema kumekuwa na mabadiliko makubwa ya viongozi wa vijiji kuhusu suala zima la usimamizi wa ardhi, kwani sasa wamekuwa wakielewa sheria zilizopo na wamekuwa wakizifuata pindi wanapotaka kuuza ardhi za vijiji.
Marwa alisema wamekuwa wakiwajengea uwezo wajumbe wa kamati za ardhi katika vijiji kwenye suala zima la utatuzi wa migogoro na usimamizi wa ardhi ya kijiji.
Alisema kwa kushirikiana na kamati hizo wamekuwa wakitekeleza mipango endelevu ili kupunguza migogoro ya ardhi.
Mradi huo umefadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), utekelezaji wake ulianza mwaka 2013 na unatarajia kukamilika mwaka 2017.
“Msingi mzima ni ushiriki wa wananchi kusimamia ardhi yao vizuri, wasiuze ardhi ni nyenzo muhimu katika kilimo na ufugaji,” alisema.
Mradi huo unatekelezwa katika vijiji vitano vya wilaya ya Bahi ambavyo ni Mpalanga, Hing’ila, Ibugile, Tinai na Kongogo. Mwitikio umekuwa mkubwa kwani vijiji vilivyokuwa na migogoro mingi sasa imepungua na kuamua kutenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Francis Mwonga alisema ni wajibu wa kiongozi kuhakikisha kunakuwa na matumizi bora ya ardhi. Alisema ardhi ni moja ya rasilimali muhimu hivyo mafunzo hayo yawajengee uelewa ili kuongeza kasi katika utendaji wao wa kila siku.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bahi, aliwataka wajumbe wanaopata mafunzo hayo wakafanye kazi kwa vitendo ili kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
“Nia yetu ni kuona mwisho wa siku migogoro inakwisha, jambo hili lilitakiwa kufanywa na halmashauri lakini wenzetu wanalifanya kuwa jambo la ajabu mwisho wa siku wasione kinachoendelea, hiyo haitaleta picha nzuri kwenye wilaya yetu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment