
MWENYEKITI wa zamani wa Klabu ya Simba Ismail Rage, amewataka viongozi waliopo madarakani kupunguza malumbano na wachezaji ili kujenga kikosi imara ambacho kitarudisha heshima ya timu hiyo kwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali watakayoshiriki yakiwemo yale ya kimataifa.
Rage alisema kufanya vibaya kwa timu hiyo kumetokana na viongozi kuwafukuza wachezaji wazuri bila sababu za msingi jambo ambalo limechangia timu hiyo kushindwa kufanya vizuri kwa sababu kila msimu timu hiyo inakuwa na idadi kubwa ya wachezaji wapya.
“Niseme ukweli kwamba Yanga ndiyo timu bora hivi sasa hapa kwetu Tanzania kwa sababu wamesajili wachezaji wazuri wenye uwezo na wamekaa pamoja kwa muda mrefu tofauti na Simba yetu ambayo kila msimu tunakuwa tukisajili wachezaji wapya ambao wamekuwa wakihitaji muda kuzoeana na wengine wamekuwa wakifukuzwa pasipo sababu za msingi,” alisema Rage.
Kiongozi huyo alisema kitu kingine ambacho kimekuwa kikwazo cha mafanikio ya Simba ni uongozi kuogopa vikao vya wanachama ambavyo kwa asilimia kubwa vinakuwa na nia njema ya watu hao kutaka kujua mwenendo wa timu yao na kuwaweka wazi namna ya uendeshwaji wa klabu yao.
Alisema wakati wa uongozi wake aliwahi kukumbana na jambo hilo mara mbili, lakini alijitahidi kuhakikisha wanachama wanapata haki yao ya msingi na kikatiba kwa kukutana nao na kusikiliza mawazo yao na aliyafanyia kazi ingawa hawakuweza kufanya vizuri katika msimu wake wa mwisho.
“Mimi nawashauri wenzangu kutanguliza busara mbele na wasiogope vikao vya wanachama pia nawatakia mafanikio mema kuelekea Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 10, mwaka huu cha msingi wajitahidi kufanya usajili mzuri msimu huu kwa kutumia pesa za usajili wa Emmanuel Okwi na Mbwana Samatta, ili kurudisha mafanikio ya Simba,” alisema.
Mara ya mwisho Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ilikuwa msimu wa 2011/12, ikiwa chini ya uongozi wa Rage tangu hapo timu hiyo imekuwa ikipambana kurudia mafanikio hayo licha ya kubadilisha uongozi kuingia Evans Aveva, lakini imekuwa ikiishia kumaliza katika nafasi ya tatu na nne.
0 comments:
Post a Comment