.

.

Kichapo kuchezea, vichura kurukishwa na mapomu kupigwa!!


MABOMU ya machozi jana yalipigwa nje ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuwatawanya mashabiki wa soka waliokuwa wakilazimisha kuingia uwanjani kushuhudia Yanga ikicheza na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mashabiki wa soka walianza kuingia uwanjani mapema asubuhi na ilipofika saa tano asubuhi tayari uwanja ulikuwa umejaa pomoni na askari walianza kuzuia watu wasiendelee kuingia uwanjani.
Sehemu ya viti vya wageni mashuhuri (VIP) pekee ndio ilikuwa na nafasi na iliachwa mahsusi kwa ajili ya wageni maalum wa timu hizo pamoja na wale wa serikali.
Lakini tukio la mashabiki kuzuiwa baadhi yao hawakukubaliana nalo, hivyo kulazimisha kuingia ndani kwa nguvu. Kutokana na hali hiyo ilibidi polisi kutumia mabomu ya machozi majira ya saa sita mchana muda mfupi baada ya kutangaziwa kwamba uwanja ulikuwa umejaa.
Licha ya tukio hilo la polisi, lakini baadhi ya mashabiki hao wengi wao wakiwa vijana waliendelea kung’ang’ania kutaka waingie uwanjani. Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alituma ujumbe katika vyombo vya habari kuomba watangaze wananchi wasiende uwanjani maana ulikuwa umejaa.
“Naomba wananchi ambao wapo njiani kuja uwanjani wasije uwanja umejaa tayari na mageti yamefungwa. Pia wale waliopo nyumbani wabaki hukohuko,” alisema Lucas majira ya saa sita mchana jana.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliingia uwanjani hapo majira ya saa 7;30 mchana kuangalia hali ya usalama na baadaye kupanda jukwaa la VIP.
Kivutio kingine kikubwa jana ilikuwa mashabiki wa TP Mazembe ambao wakati wanaingia uwanjani walishangiliwa kwa kiasi kikubwa na mashabiki wa Simba. Mashabiki wa Yanga walijitahidi kwa kiasi kikubwa kuihamasisha timu yao jana kwa kuishangilia kwa nguvu, lakini matokeo hayakuwa mazuri kwa upande wao.
Share on Google Plus

About UPStream Telecom

0 comments:

Post a Comment