Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
MAREKEBISHO ya Sheria mpya ya Manunuzi, yamewasilishwa bungeni
yakitamka kufyeka posho za watendaji, wanaosimamia mchakato wa zabuni na
kuondoa vikao vya bodi kutoka 12 kwa mwaka hadi vinne, ikisisitiza
kuziba mianya ya rushwa na kuongeza uwazi.
Aidha, muswada wa marekebisho hayo, unataka kampuni au mshauri wa nje
ili apewe zabuni katika shughuli zinazogharimiwa na fedha za umma,
ahakikishe asilimia 60 ya wafanyakazi wa kampuni yake ni Watanzania.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, aliyasema hayo jana
mjini hapa wakati akiwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2016.
Kupungua kwa vikao vya bodi, kumeelezwa na Dk Mpango kuwa kutapunguza
gharama zinazotokana na posho ya vikao vya bodi ya zabuni na ada
zinazolipwa kwa kamati zinazohusika na mchakato ya zabuni.
Aidha, posho zinazotokana na utekelezaji wa majukumu ya kazi ya kila
siku ya washiriki itafutwa. Hata hivyo, imeruhusu kuwapo kwa vikao vya
dharura pale Mwenyekiti wa Bodi akiona ni lazima.
Pamoja na kupunguzwa vikao, muda wa zabuni nao umepunguzwa na pia
taasisi nunuzi itaruhusiwa kufanya majadiliano ya bei wakati wa mchakato
wa zabuni kwa lengo la kupunguza bei ya ununuzi na kuongeza bei ya
kuuza mali za serikali.
Dk Mpango alisema sheria hiyo mpya, itaziba mianya ya rushwa,
kuongeza kasi, uwazi, uwajibikaji na kuleta upendeleo maalumu kwa
kampuni za Tanzania katika zabuni za ndani na za kimataifa.
Pia sheria hiyo itaongeza ufanisi na kupata thamani halisi ya fedha, inayotumika kwa kununua huduma na bidhaa.
Dk Mpango alisema pamoja na kuongeza uwajibikaji, sheria hiyo mpya
itapunguza vikao vya bodi hadi kuwa kimoja kwa robo mwaka na vikao vya
dharura, kufanyika pale ambapo mwenyekiti ataona inabidi.
Pamoja na maelekezo hayo mapya, serikali pia itaanza kununua bidhaa
na huduma kwa bei inayoendana na bei ya soko, iwapo wabunge watapitisha
marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma.
Pamoja na ununuzi wa bei ya soko, sheria mpya imelenga kuweka sharti
la kisheria kutoa upendeleo katika zabuni mbalimbali, hasa kwa makundi
maalumu kama vile wanawake, vijana, wazee na watu wenye mahitaji
maalumu.
Alieleza kuwa sheria mpya imelenga kuiwezesha serikali, kunufaika na
matumizi ya viwango na kuweka sharti la kisheria la kutumia mifumo ya
kuongeza uwazi katika ununuzi ili kuongeza uadilifu na uwajibikaji.
Kwa mujibu wa waziri, sheria mpya imelenga kurahisisha ununuzi wa
umma na kuipa faida serikali baada ya kuwapo kwa changamoto nyingi kwa
Sheria Namba 7 ya Mwaka 2011, ambayo ilianza kutekelezwa mwaka huo.
Changamoto hizo ni pamoja na bei ya juu ya bidhaa na huduma
zinazonunuliwa na serikali kulinganisha na bei ya soko kutokana na zuio
la majadiliano kuhusu bei kati ya taasisi nunuzi na mzabuni.
Pamoja na changamoto ya bei, kumekuwepo na muda mrefu wa mchakato,
gharama kubwa zinazotokana na matangazo na vikao mbalimbali vya kupitia
zabuni, kutozingatiwa kwa viwango na kutokuwepo kwa upendeleo katika
ushiriki wa zabuni kwa makundi maalumu.
Mapendekezo ya muswada huo, pia yametaka pale kampuni au taasisi ya
umma inapolazimika kufanya ununuzi kutoka nje ya nchi, hasa kama ni
suala la ushauri linafanywa na kampuni ya nje ya nchi, ofisi hiyo ya
serikali inalazimika kuhakikisha kuna wataalamu wa ndani ya nchi.
Aidha, kampuni au mshauri huyo wa nje ili apewe zabuni katika
shughuli ambazo zinagharimiwa na fedha za umma, kuna kigezo cha
kuhakikisha wafanyakazi wa kampuni yake, zaidi ya asilimia 60 ni
Watanzania.
Mbali na kuwa na asilimia 60 ya wafanyakazi Watanzania, kampuni
husika lazima ieleze kiwango cha bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani
ya nchi, ambazo itazinunua katika utekelezaji wa shughuli zake.
Nayo Kamati ya Bunge ya Bajeti imeitaka serikali kusimamia na
kuhakikisha kwamba watumishi wa umma ambao hawastahili kupewa magari,
watumie magari yao binafsi ; na wale ambao wanastahili wakopeshwe magari
na serikali na kupewa posho kidogo kwa ajili ya mafuta na matengenezo.
Pia, imeitaka serikali iandae utaratibu wa kununua magari kwa pamoja yasiyo na gharama kubwa kulingana na bei ya soko.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Bajeti kuhusu Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2016, Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Hawa Ghasia alisema kamati imekubaliana na serikali kufanya
manunuzi kwa kuzingatia thamani ya fedha kwa bidhaa, ikiwamo manunuzi
ya magari Alisema muswada huo unaonesha kwamba inawezekana kupunguza
gharama za serikali kwa kufuata thamani ya fedha.
Aidha kamati hiyo imeishauri serikali kuanzisha mfuko wa uwezeshaji
wa makandarasi ili waweze kumudu utoaji wa huduma mbalimbali,
zinazohuisha gharama kubwa, mfano ukandarasi wa barabara. Mfuko huo
utakuwa ukitoa dhamana. Pia kamati hiyo inataka kujua mwanzo wa matumizi
ya sheria mpya.
Wabunge waliochangia muswada huo, waliitaka serikali nayo kujiunga
katika sheria hiyo kwa kuona kwamba inawalipa wazabuni mapema au
inaeleza watakavyoweza kuwa wazabuni wanapochelewesha malipo, hasa
kutokana na kampeni yake ya ununuzi kwa bei ya soko.
Wabunge hao walisema kwamba serikali inajua sababu za bei kubwa na
hivyo inafaa ikajipanga kuondoa kasoro hiyo ili hiyo sheria iweze
kutekelezeka.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Ligora (CCM) alitoa tahadhari kwamba sheria
inabadilishwa Ibara 40 ambayo ni sehemu kubwa na kusema kwamba lazima
ijiandae kuondoa sababu za bei kubwa na pia kutofuta kipengele cha
kamati ya mipango na fedha kwenye halmashauri kupitia zabuni kwa lengo
la kujiridhisha.
Kauli ya kutofuta kipengele hicho katika muswada, pia ilizungumzwa na wabunge waliochangia jana.
Aidha wengine walitaka kuwapo na dirisha kwa ajili ya dharura na hasa
dirisha kwa ajili ya bidhaa za afya na tiba. Wabunge wengine
waliochangia ni Martha Mlata, Rita Kabati, Ali Hassan, Dk Diodorus
Kamara, Japhet Asunga, Adadi Rajab, Jitu Son, John Kadutu na Amina
Mollel.

0 comments:
Post a Comment