Rais wa
shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck amesema umri wake ndio
chanzo cha kuamua asigombee mhula wa pili mwezi februari mwaka 2017.
Akizungumza na waandishi habari katika kasri lake la Bellevue mjini
Berlin rais Joachim Gauck ambae hivi sasa ana umri wa miaka 76
amesema:"Leo nnapendelea kukuarifuni kwamba nimeamua,nisipiganie tena
mhula mwengine wa rais wa shirikisho. Uamuzi huo haukuwa rahisi
kwangu,kwasababu ni heshima kubwa kwangu kupata fursa ya kuitumikia nchi
hii,nchi yetu,shirikisho la jamhuri ya Ujerumani."
Hata kama
wadhifa wake kwa sehemu kubwa ni wa heshima,kuanzia uongozi wa
kimaadili na kuiwakilisha Ujerumani nchi za ng'ambo,Gauck,aliyechaguliwa
mwaka 2012 kwa mhula wa miaka mitano,hakuchelea kuchukua msimamo katika
jukwaa la ndani la kisiasa,naiwe kwa kuunga mkono sera za kuwapokea
wakimbizi au kwa kuzungumzia majukumu ya kihistoria ya nchi hii.
Kinyang'anyiro cha nani awe rais wa shirikisho kinaanza
Kwa
kutangaza rasmi uamuzi wake ambao vyombo vya habari vimekuwa tangu siku
kadhaa sasa vikiashiria,analifungulia njia "Baraza la shirikisho"pale
wabunge wa shirikisho na wawakilishi wa mabaraza ya majimbo
watakapokutana kumchagua mtu atakaeshika nafasi yake mwezi Februari
mwakani.
Kwasasa
hakuna chama chochote chenye wingi mkubwa kuweza kumchagua mgombea
wake,inamaanisha pengine duru tatu za uchaguzi zitahitajika hadi rais
mpya atakapochaguliwa. Zoezi hilo la uchaguzi linaashiria pia malumbano
makali katika wakati ambapo kila chama tayari kimeanza kujiandaa kwa
uchaguzi mkuu wa msimu wa mapukutiko mwakani na ambao kansela Angela
Merkel bado hajatangaza dhamiri yake.
Kansela
Angela Merkel atakaekutana baadae hii leo na rais wa shirikisho Joachim
Gauck,anaweza kuchagua mgombea ama kutoka vyama ndugu vya CDU/CSU au
kumtafuta mtu mwenye nafasi nzuri ya kuungwa mkono na vyama vyingi vya
kisiasa. Majina kadhaa yamekuwa yakitajwa na vyombo vya habari ikiwa ni
pamaoja na spika wa bunge la shirikisho, Bundestag, Norbert Lammert wa
chama cha CDU na waziri wa fedha Wolfgang Schäuble.
Mwanamke wa kwanza kuwa rais wa shirikisho
Kansela
Merkel anaweza pia kumgeukia Gerda Hasselfeldt wa chama cha CSU na kwa
namna hiyo kuwa sababu ya kutuliza mvutano wa miezi kadhaa pamoja na
chama hicho cha kusini mwa Ujerumani. Jina jengine la mwanamke
linalotajwa ni lile la waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen,lakini
wadadisi wanaamini lengo lake ni kuweza siku moja kumrithi kansela
Angela Merkel.
Wadhifa
wa rais wa shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani ni wa heshima. Anaweza
kuchaguliwa tena mara moja tu. Raia yeyote mwenye umri wa zaidi ya miaka
40 anaweza kugombea wadhifa huo.DW
0 comments:
Post a Comment