.

.

Penalti ya samatta ilitugharimu, asema kocha

Mshambuliaji wa taifa stars Mbwana samatta
KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ Charles Mkwasa alisema penalti waliyokosa katika mchezo dhidi ya Mafarao wa Misri ilipoteza mwelekeo wa timu hiyo kufanya vizuri.
Alisema pia, Misri walistahili kushinda kutokana na uwezo mkubwa waliouonesha katika safu zao zote lakini pia, walionekana kucheza mpira kwa nidhamu na ufundi mkubwa. Katika mchezo huo uliochezwa juzi, Taifa Stars iliaga rasmi mbio za kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kipigo cha mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2017) zitafanyika Gabon mwakani na Misri imefuzu kutoka katika kundi hilo la G. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo Mkwasa alisema baada ya Mbwana Samatta kukosa penalti waliyopata kipindi cha pili cha mchezo huo, timu ilipoteza mwelekeo na kuipa nafasi Misri kucheza kwa kujiamini na kufanikiwa kupata bao la pili.
Taifa Stars ilipata penalti dakika 53 baada ya Himid Mao kuchezewa rafu ndani ya eneo la hatari na Amr Mohsen aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mohamed Ibrahim. “Tulivyopanga imekuwa tofauti, timu ilikwenda vizuri mwanzoni lakini baadaye ikapoteza nafasi kidogo, wenzetu walicheza vizuri kwa nidhamu na walikuwa na nguvu na tatizo letu tulitoka zaidi baada ya kupoteza penalti, kisaikolojia iliwasaidia wenzetu kupambana zaidi na kupata bao la pili,” alisema.
Mkwasa alisema licha ya kutolewa, vijana wake walijitahidi kwa uwezo wao lakini walizidiwa hivyo hawana budi kujipanga upya kwa wakati ujao. Alisema bado wako kwenye mchakato wa kujenga timu na ana imani vijana hao wanaweza kama wataendelea kuandaliwa na kutengenezwa hasa kwa wale ambao watakuwepo.
“Kwa matokeo tuliyoyapata tayari tumepoteza tumaini hata tutakapoenda kukutana na Nigeria hatuwezi kusonga mbele, awali tuliamini kama tungeshinda tungeenda kule kushindana lakini hata kama tutaenda kupata matokeo mazuri hatuwezi kusonga mbele kwa kuwa wenzetu wamefuzu kwa pointi 10 ambazo hakuna anayeweza kuzifikia,” alisema.
Share on Google Plus

About UPStream Telecom

0 comments:

Post a Comment